Jumatatu 4 Mei 2026 - 11:15
Sheikh Qablan alisema nini katika barua yake kali kumuelekea Rais wa Lebanon?

Hawza/ Mufti wa Ja‘fari mashuhuri na mwanazuoni wa Kishia wa Lebanon, katika barua ya wazi aliyomwandikia Joseph Aoun, alibainisha kuwa; Lebanon inashikamana na hati yake ya kitaifa na misingi yake ya kimaadili.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad Qablan, Mufti wa Ja‘fari na mwanazuoni mashuhuri wa Kishia wa Lebanon, katika barua ya wazi kwa Joseph Aoun, alisema: Kwa msingi wa maslahi ya taifa na uwiano wake ulio wazi, ninamwambia Rais kwamba; Lebanon inashikamana na hati yake ya kitaifa na misingi ya maadili. Katiba ya Lebanon inajumuisha misingi na kanuni za kitaifa pamoja na mambo ya makubaliano yanayolinda maslahi na masuala ya hatima ya Lebanon. Nje ya hayo, hakuna nguvu yenye thamani ikiwa inakwenda kinyume na misingi hiyo thabiti, na makubaliano ya Aprili 17 ni mfano hai wa ukweli huu wa kudumu.

Aliongeza kuwa: Lebanon ni nchi inayokabiliwa na vitisho na ina haki ya kujilinda na kuimarisha uwezo wake wa kitaifa—jambo ambalo Washington na Tel Aviv hawalitaki. Marekani hufanya mambi kwa kuzingatia kikamilifu maslahi ya Israel katika eneo. Wakati Israel ilipoiteka Beirut, Washington ilituma vikosi vyenye nguvu vya kimataifa nchini Lebanon, na Lebanon iliweza kujinasua tu kupitia mapambano ya muqawama, hasa chini ya uongozi wa kihistoria wa Nabih Berri, ambaye aliongoza mapinduzi ya tarehe 6 Februari. Leo hali ni mbaya zaidi, na Marekani ndio chanzo cha migogoro duniani na eneo, na ndiye mhusika mkuu wa mauaji ya Israel huko Palestina, vita vya eneo na uhalifu uliofanyika katika kile kinachoitwa “Masika ya Kiarabu”, na hata katika mazungumzo yake mapya na Iran inaonyesha wazi kuwa Marekani kiasili ni adui.

Leo vita vyote vya eneo vya Israel vinaendeshwa na Washington

Sheikh Qablan aliendelea kusema: Leo vita vyote vya eneo vya Israel vinaendeshwa na Washington, na hili mnalijua. Mipango mikubwa ya Israel ni mipango ya kijeshi ya Marekani, na hapa ndipo kuna hatari kubwa. Mantiki ya vita vyote—na vita hii ya hatima—imejengwa juu ya msingi huo. Miongoni mwa shinikizo la Marekani kwa serikali ya Lebanon ni kulazimisha mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wa Israel, ilhali nguvu ya Lebanon imedhoofika na serikali haina uwezo wala hadhi; jambo hili ni dalili ya udhaifu na fedheha ya nchi, huku Benjamin Netanyahu akinufaika.

Sheikh Qablan alisisitiza: Hakuna mwenye akili timamu na mwenye mapenzi ya nchi anayeweza kukubali hali hii. Suala si nia bali ni vitendo. Na mantiki ya vitendo inaonyesha wazi kwamba; serikali ya Lebanon, ilipoingia katika mazungumzo ya moja kwa moja na utawala vamizi wa Israel, imejichinja yenyewe. Sababu za jambo hili ni nyingi na ziko nje ya misingi ya itikadi ya kitaifa. Miongoni mwazo ni kwamba; bila muqawama, serikali ya Lebanon haina tena nguvu, hadhi, uwezo wa uwakilishi wala uwezo wa kuzuia. Hili ni suala la kitaifa linalohusu mikataba na gharama za mamlaka, ambalo linapita mbali zaidi ya mitazamo ya mgawanyiko. Hali ya uwanjani imeonyesha—kinyume na dhana ya awali—kwamba Israel yenyewe imeingia katika mtego wa kimkakati, na leo jeshi lake liko katika hali ya kusitasita na haliwezi kudhibiti mazingira, huku uwezo wake wa kijeshi ukidhoofika.

Aliongeza kuwa: Nilishakushauri hapo awali kwamba; ukipoteza akili na fikra za Nabih Berri, utaipoteza Lebanon pia. Suala si jina bali ni nafasi, uwezo na uongozi wa mtu huyu katika kudhibiti ushawishi wa Israel na kupunguza utawala wa Marekani. Lengo lake si madaraka bali ni umoja wa kitaifa na mshikamano wa Kiislamu na Kikristo, na kulinda uhuru wa nchi. Mantiki yake inaweza kufupishwa kwa kauli hii: mwakilishi rasmi akichota nguvu kutoka kwa kundi moja tu, huipoteza Lebanon. Na yeyote anayepuuza uhusiano wa kitaifa na kuingia katika masuala ya hatima hupoteza nafasi yake.

Hatutaitambua dola iliyojengwa juu ya mauaji

Mwanazuoni huyu wa Kishia alimwambia Rais kuwa: Lebanon ni amana ya historia na ya Mwenyezi Mungu, na kulinda amana hii hakuwezi kupatikana kupitia mazungumzo ya moja kwa moja na muuaji wa Mitume na adui wa mataifa (Israel). Hatuwezi kuitambua dola iliyojengwa juu ya miili ya Wapalestina na juu ya mauaji ya Lebanon, hata kama dunia yote itaitambua. Hii si kauli tupu bali ni kwa sababu muqawama umeonesha uwezo wa kipekee katika kulinda mamlaka ya taifa. Muqawama ni ngao imara ya Lebanon sambamba na jeshi la taifa.

Muqawama ulilazimika kuingia uwanjani kutokana na udhaifu wa serikali

Sheikh Qablan aliendelea kusema: Muqawama katika vita hii na vita nyingine haukupigana kwa maslahi ya nje, bali uliingia uwanjani kwa sababu mamlaka ya Lebanon ilishindwa kulinda nchi dhidi ya mashambulizi ya kila siku ya Kizayuni. Hivyo, kuilinda Lebanon, kuzuia mikataba yenye shaka na kuupiga uwezo wa kijeshi wa Israel lilikuwa ni jambo lisiloepukika.

Alisisitiza kuwa: Leo uwezo wa kuzuia wa Israel unavunjwa kwa mashambulizi ya kisasa, hali iliyomlazimisha Benjamin Netanyahu kukimbilia Washington kuomba msaada, ili kuishinikiza serikali ya Lebanon ichukue hatua dhidi ya muqawama kwa mujibu wa hati hatari ya Marekani.

Alionya kuwa; hatari ya hati hiyo ni kuweka jeshi la Israel mikononi mwa mamlaka ya Lebanon ili kuvunja silaha za muqawama—hali ambayo ni fedheha kubwa, hasa kwa kuwa muqawama kwa karibu nusu karne umeilinda Lebanon.

Hakuna umoja wa kitaifa pamoja na mazungumzo ya aibu na Israel

Sheikh Qablan alisema: Leo ni wakati wa umoja wa kitaifa kwa ajili ya kuilinda Lebanon, si kupuuza uvamizi na uharibifu wa Israel. Hakuna umoja wa kitaifa unaoweza kuwepo pamoja na mazungumzo ya moja kwa moja ya aibu na Israel, na uhalali uko katika kuipinga Israel, si katika kujadiliana nayo.

Alisisitiza kuwa; wananchi wa kusini, Dhahieh na maeneo mengine wana haki ya kuuliza sababu ya anguko hili la kisiasa na chaguzi hizi za fedheha, pamoja na kushindwa kwa serikali kutekeleza wajibu wake wa kitaifa.

Umuhimu wa kupambana na Israel na kuifukuza kutoka maeneo ya mbele

Alisema kwamba: Kwa kuwa huu ni wakati wa maslahi ya taifa, na kwa kuwa Israel inapoteza mafanikio yake ya vita vya zamani, Rais anapaswa kuanzisha mpango wa kitaifa unaojengwa juu ya umoja wa Lebanon, hasa katika masuala ya hatima na mipaka, na kusisitiza ulazima wa kupigana na Israel, kuifukuza kutoka maeneo ya mbele na kuweka jeshi la Lebanon katika mipaka yote—kwa sharti la kusitisha mazungumzo ya moja kwa moja.

Alimalizia kwa kusema: Rais anapaswa kutekeleza wajibu wake wa kitaifa, kulinda nchi na kutangaza uhamasishaji wa kitaifa dhidi ya adui wa Kizayuni ambaye tangu mwaka 1948 ameendelea na vita dhidi ya Lebanon. Wajibu wa kitaifa ni kuilinda Lebanon, si kuhalalisha uvamizi. Rais anatakiwa kulitazama suala la Israel kwa macho ya watu wa kusini, kwa hekima na historia ya Nabih Berri, na kwa mwamko wa tarehe 6 Februari pamoja na fikra za waanzilishi waliokuwa wakionya dhidi ya mradi wa Marekani wa kuigeuza Lebanon kuwa ya Kizayuni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha